Print this page
2 HOURS AGO
Wahalifu wa kimtandao wavamia tovuti ya Chuo Kikuu Huria Waingilia mawasiliano ya tovuti na kuandika ujumbe wa vitisho. Kwa ufupi
Dk Nfuka amesema kilichotokea ni changamoto inayotokana na ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano.
Kelvin Matandiko, Mwananchi
[email protected] Dar es Salaam. Wahalifu wa kimtandao wamezua taharuki baada ya kuingilia mawasiliano ya tovuti ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT). Wakijitambulisha kwa jina la Tanzania Hackers kwa saa kadhaa wahalifu hao waliingilia mawasiliano ya tovuti hivyo na kuacha ujumbe wa mahitaji ya ajira kwa nguvu, wakisema kinyume cha hilo wataingilia mifumo ya Serikali. Mmoja wa watumishi chuoni hapo aliyeomba kuhifadhiwa jina leo Jumatano Oktoba 25,2017 amesema wameshindwa kufanya kazi asubuhi hadi saa 10:00 jioni wakati uongozi wa chuo ukiendelea na jitihada za kuirejesha tovuti hiyo katika mfumo wa awali. Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Mawasiliano (IT) chuoni hapo, Dk Edephonce Nfuka amekiri kutokea kwa shambulio hilo la kimtandao. “Tumeliona tatizo asubuhi lakini tuliweka mfumo mbadala. Tunashukuru TCRA Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania nao walipoliona tatizo hilo wakatujulisha,” amesema Dk Nfuka. Amesema baada ya tukio hilo alitoa taarifa kwa Wakala wa Serikali Mtandao (eGovernment Agency) ili wachukue tahadhari kutokana na vitisho vilivyotolewa na wahalifu hao.
“Wamesema wamejiweka sawa kwa uhalifu wowote utakaojitokeza, wako vizuri,” amesema. Kuhusu kilichotokea, Dk Nfuka amesema ni changamoto inayotokana na ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano. Amekemea vijana wanaopata taaluma ya IT kuitumia katika matukio ya uhalifu. Baada ya kuingilia tovuti hiyo, wahalifu hao wameeleza kuchukizwa na hali ya kuishi maisha ya bila ajira huku wakiwa na taaluma hiyo. Kuhusu uhalifu huo wa mtandao, Kaimu Meneja Mawasiliano wa TCRA, Semu Mwakyanjala amesema unapotokea mamlaka hupokea malalamiko kutoka kwa aliyeathiriwa au Jeshi la Polisi kikosi cha kudhibiti uhalifu wa kimtandao. Amesema kikosi hicho ndani ya Jeshi la Polisi ndicho hufuatilia wizi wa kwenye mashine za ATM na ujambazi wa kutumia teknolojia. Mwakyanjala amesema kikosi hicho kinapohitaji msaada wa TCRA wao hutoa ufumbuzi.